Mit. 14 SUV

1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake;Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

2 Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA;Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.

3 Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi,Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.

4 Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe;Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi.

5 Shahidi mwaminifu hatasema uongo;Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.

6 Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate;Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.

7 Toka mbele ya uso wa mpumbavu,Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.

8 Akili za mwenye busara ni kujua njia yake;Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.

9 Wapumbavu huidharau hatia;Bali upo upendeleo kwa wenye haki.

10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake,Wala mgeni haishiriki furaha yake.

11 Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa;Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.

12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

13 Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni;Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.

14 Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe;Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.

15 Mjinga huamini kila neno;Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.

16 Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu;Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.

17 Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga;Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.

18 Wajinga hurithi upumbavu;Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.

19 Wabaya huinama mbele ya wema,Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.

20 Maskini huchukiwa hata na jirani yake;Bali tajiri ana rafiki wengi.

21 Amdharauye mwenzake afanya dhambi;Bali amhurumiaye maskini ana heri.

22 Je! Hawakosi wawazao mabaya?Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.

23 Katika kila kazi mna faida;Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.

24 Taji ya wenye hekima ni mali zao;Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.

25 Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu;Bali atoaye uongo hudanganya.

26 Kumcha BWANA ni tumaini imara;Watoto wake watakuwa na kimbilio.

27 Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima,Ili kuepukana na tanzi za mauti.

28 Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake;Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.

29 Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi;Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.

30 Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili;Bali husuda ni ubovu wa mifupa.

31 Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake;Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.

32 Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake;Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.

33 Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu;Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.

34 Haki huinua taifa;Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31