Mit. 18 SUV

1 Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe;Hushindana na kila shauri jema.

2 Mpumbavu hapendezwi na ufahamu;Ila moyo wake udhihirike tu.

3 Ajapo asiye haki, huja dharau pia;Na pamoja na aibu huja lawama.

4 Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi;Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima.

5 Kukubali uso wake asiye haki si vizuri;Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni.

6 Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina,Na kinywa chake huita mapigo.

7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake,Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake.

8 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo;Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.

9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake,Ni ndugu yake aliye mharabu.

10 Jina la BWANA ni ngome imara;Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.

11 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu;Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.

12 Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna;Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

13 Yeye ajibuye kabla hajasikia,Ni upumbavu na aibu kwake.

14 Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake;Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?

15 Moyo wa mwenye busara hupata maarifa;Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.

16 Zawadi ya mtu humpatia nafasi;Humleta mbele ya watu wakuu.

17 Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki;Lakini jirani yake huja na kumchunguza.

18 Kura hukomesha mashindano;Hukata maneno ya wakuu.

19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu;Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.

20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake;Atashiba mazao ya midomo yake.

21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi;Na wao waupendao watakula matunda yake.

22 Apataye mke apata kitu chema;Naye ajipatia kibali kwa BWANA.

23 Maskini hutumia maombi;Bali tajiri hujibu kwa ukali.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31