Mit. 28 SUV

1 Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu;Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2 Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi;Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa

3 Mtu mhitaji awaoneaye maskini,Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.

4 Wao waiachao sheria huwasifu waovu;Bali wao waishikao hushindana nao.

5 Watu wabaya hawaelewi na hukumu;Bali wamtafutao BWANA huelewa na yote.

6 Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake,Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.

7 Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima;Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.

8 Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida,Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

9 Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria,Hata sala yake ni chukizo.

10 Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya,Ataanguka katika rima lake mwenyewe;Bali wakamilifu watarithi mema.

11 Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe;Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.

12 Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi;Bali waovu waondokapo, watu hujificha.

13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

14 Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote;Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.

15 Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa;Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.

16 Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana;Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.

17 Aliyelemewa na damu ya mtuAtalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.

18 Aendaye kwa unyofu ataokolewa;Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.

19 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.

20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele;Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.

21 Kupendelea watu si kwema;Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.

22 Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri;Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.

23 Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali;Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.

24 Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa;Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.

25 Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina;Bali amtumainiye BWANA atawandishwa.

26 Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga;Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.

27 Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu;Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31