17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki;Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga;Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele;Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu;Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote;Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA;Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa;Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.