1 Mwanangu, sikiliza hekima yangu;Tega sikio lako, mzisikie akili zangu;
2 Upate kuilinda busara,Na midomo yako iyahifadhi maarifa.
3 Maana midomo ya malaya hudondoza asali,Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
4 Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga;Ni mkali kama upanga wa makali kuwili.
5 Miguu yake inatelemkia mauti;Hatua zake zinashikamana na kuzimu;
6 Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima;Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.