1 Hata ikawa baada ya siku nyingi, BWANA alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana,
2 Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu;
3 nanyi mmeona mambo yote ambayo BWANA, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi.
4 Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua.
5 Yeye BWANA, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama BWANA Mungu wenu, alivyowaambia.
6 Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto.
7 Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao;