15 Samueli akamwambia Shauli, “Kwa nini unanisumbua kwa kunileta juu?” Shauli akamjibu, “Mimi nina taabu kubwa! Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, na Mungu amenipa kisogo; hanijibu tena kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Ndio maana nimekuita unijulishe la kufanya.”
16 Samueli akasema, “Kwa nini unaniomba shauri ambapo Mwenyezi-Mungu amekupa kisogo na amekuwa adui yako?
17 Mwenyezi-Mungu amekutendea kile alichokuambia kwa njia yangu. Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, na amempa Daudi jirani yako.
18 Maana, wewe hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, wala hukuitekeleza ghadhabu yake dhidi ya Waamaleki. Ndio maana leo Mwenyezi-Mungu amekutendea mambo haya.
19 Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakutia wewe pamoja na Waisraeli wote mikononi mwa Wafilisti. Kesho, wewe na wanao mtakuwa pamoja nami; hata jeshi la Israeli Mwenyezi-Mungu atalitia mikononi mwa Wafilisti.”
20 Ghafla, Shauli akiwa na hofu kutokana na maneno ya Samueli, alianguka kifudifudi; hakuwa na nguvu zozote; kwa kuwa alikuwa hajala chochote kwa siku nzima, usiku na mchana.
21 Ndipo yule mwanamke alipomwendea Shauli, na alipoona kuwa Shauli ameshikwa na hofu mno, alimwambia, “Mimi mtumishi wako nimehatarisha maisha yangu kwa kufanya kile ulichoniambia nikufanyie.