11 Wale watu waliokuwa na Daudi walimkuta mtu mmoja Mmisri nyikani, nao wakampeleka kwa Daudi. Wakampa mtu huyo mkate na maji.
12 Pia walimpa kipande cha mkate wa tini na vishada viwili vya zabibu kavu. Alipomaliza kula, akapata nguvu, kwani alikuwa hajala wala kunywa kitu chochote kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku.
13 Daudi akamwuliza, “Bwana wako ni nani? Na umetoka wapi?” Yeye akamwambia, “Mimi ni kijana Mmisri. Ni mtumishi wa Mmaleki mmoja. Bwana wangu aliniacha nyuma siku tatu zilizopita kwa kuwa nilikuwa mgonjwa.
14 Sisi tulishambulia sehemu ya jangwa wanamoishi Wakerethi, eneo la Yuda pamoja na sehemu ya jangwa unakoishi ukoo wa Kalebu, tukauteketeza kwa moto mji wa Siklagi.”
15 Daudi akamwuliza, “Je, utaweza kunipeleka kwenye genge hilo?” Kijana akamjibu, “Ikiwa utaniapia kwa jina la Mungu kuwa hutaniua, wala kunitia mikononi mwa bwana wangu, nitakupeleka.”
16 Yule kijana alimwongoza Daudi hadi genge lile lilipokuwa. Walipofika huko waliwakuta wateka nyara hao wakiwa wametawanyika kila mahali kwani walikuwa wakila na kunywa kwa sababu nyara walizoteka kutoka nchi ya Wafilisti na nchi ya Yuda zilikuwa nyingi sana.
17 Daudi aliwapiga tangu asubuhi hadi siku ya pili jioni. Hakuna mwanamume yeyote aliyenusurika isipokuwa vijana 400 ambao walipanda ngamia na kukimbia.