4 Nilipotazama niliona upepo wa dhoruba unavuma kutoka kaskazini: Kulikuwa na wingu kubwa lililozungukwa na mngao, na moto ulichomoza humo mfululizo na katikati ya huo moto kulikuwa na kitu kinametameta kama shaba.
5 Kutoka humo nilibainisha viumbe hai wanne, ambao walionekana hivi: Walikuwa na umbo la binadamu.
6 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne.
7 Miguu yao ilikuwa imenyoka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa.
8 Walikuwa na mikono ya binadamu chini ya mabawa yao katika pande zao nne.
9 Ncha za mabawa yao ziligusana kila bawa na bawa lingine. Waliposogea, upande wowote ule, walikwenda mbele moja kwa moja bila kugeuza miili yao.
10 Kuhusu nyuso zao nne kila mmoja wao alikuwa na uso wa binadamu upande wa mbele, uso wa simba upande wa kulia, uso wa ng'ombe upande wa kushoto, na uso wa tai upande wa nyuma.