6 “Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tubuni, na kuacha kuziabudu sanamu zenu za miungu. Acheni kufanya machukizo.
7 Wakati wowote mmojawapo wa Waisraeli au mgeni yeyote akaaye katika Israeli, anapojitenga nami na kuanza kuziabudu sanamu za miungu kwa bidii na dhambi hiyo ikawa kizuizi kati yangu naye, halafu akamwendea nabii ili kujua matakwa yangu, basi, mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe, nitamjibu mtu huyo.
8 Nitapambana naye. Nitamfanya kuwa ishara na kielelezo; nitamwondoa kabisa kutoka taifa langu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
9 Na ikiwa nabii huyo atadanganyika akasema kitu, basi mimi Mwenyezi-Mungu nimempotosha. Nami nitanyosha mkono wangu kumwondoa nabii huyo kutoka kwa watu wangu wa Israeli.
10 Nitamwadhibu huyo nabii pamoja na huyo mtu aliyekuja kumwuliza matakwa yangu; wote watapata adhabu ileile,
11 ili watu wa Israeli wasiniache tena na kujichafua wenyewe kwa kutenda dhambi; ili wawe watu wangu nami niwe Mungu wao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
12 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: