18 Lakini baba yake, kwa sababu alitoza bei isiyo halali na kumwibia ndugu yake, wala hakuwatendea ndugu zake wema, hakika atakufa kwa sababu ya uovu wake.
19 “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mtoto asiadhibiwe kwa sababu ya dhambi za baba yake?’ Mtoto akitenda yaliyo ya haki na sawa, kama akiwa mwangalifu kuzingatia kanuni zangu zote, basi, huyo hakika ataishi.
20 Atakayetenda dhambi ndiye atakayekufa. Mtoto hatawajibika kwa uovu wa baba yake, wala baba hatawajibika kwa uovu wa mtoto wake. Uadilifu wa mwadilifu utamfaa yeye mwenyewe: Na uovu wa mwovu ataubeba yeye mwenyewe.
21 “Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake zote alizotenda, kama akishika kanuni zangu zote, akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa.
22 Makosa yake yote aliyofanya hayatakumbukwa; kwa sababu ya uadilifu wake ataishi.
23 Je, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nafurahia kufa kwake mtu mwovu? La hasha! Mimi napendelea aachane na njia zake mbaya apate kuishi.
24 “Lakini, mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akatenda uovu na kufanya machukizo yaleyale anayofanya mtu mwovu, je, huyo ataishi? La! Matendo yake yote mema aliyotenda hayatakumbukwa tena; atakufa kwa sababu ya uasi na dhambi aliyotenda.