20 Atakayetenda dhambi ndiye atakayekufa. Mtoto hatawajibika kwa uovu wa baba yake, wala baba hatawajibika kwa uovu wa mtoto wake. Uadilifu wa mwadilifu utamfaa yeye mwenyewe: Na uovu wa mwovu ataubeba yeye mwenyewe.
21 “Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake zote alizotenda, kama akishika kanuni zangu zote, akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa.
22 Makosa yake yote aliyofanya hayatakumbukwa; kwa sababu ya uadilifu wake ataishi.
23 Je, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nafurahia kufa kwake mtu mwovu? La hasha! Mimi napendelea aachane na njia zake mbaya apate kuishi.
24 “Lakini, mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akatenda uovu na kufanya machukizo yaleyale anayofanya mtu mwovu, je, huyo ataishi? La! Matendo yake yote mema aliyotenda hayatakumbukwa tena; atakufa kwa sababu ya uasi na dhambi aliyotenda.
25 “Lakini nyinyi mwasema, ‘Hicho afanyacho Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Sikilizeni sasa, enyi Waisraeli: Je, ninachofanya mimi si sawa? Mnachofanya nyinyi ndicho kisicho sawa.
26 Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake na kutenda uovu atakufa kwa ajili hiyo; atakufa kwa sababu ya uovu aliotenda.