14 Je, utaweza kustahimili kuwa hodari siku nitakapopambana nawe? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema na nitayatekeleza hayo.
15 Nitakutawanya kati ya mataifa na kukutupatupa katika nchi nyingine. Nitaukomesha uchafu ulioko kwako.
16 Utajiweka najisi mbele ya mataifa mengine, lakini utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
17 Tena neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:
18 “Wewe mtu! Waisraeli wamekuwa kwangu kama takataka. Wao ni kama takataka inayosalia wakati madini ya shaba, bati, chuma au risasi yanaposafishwa.
19 Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa nyinyi nyote mmekuwa takataka ya madini, mimi nitawakusanya pamoja mjini Yerusalemu.
20 Kama watu wanavyokusanya fedha, shaba, chuma, risasi na bati katika tanuri ili kuzisafisha kwa kuchoma moto, ndivyo ghadhabu na hasira yangu itakavyowakusanya huko na kuwayeyusha.