3 Uambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe ni mji unaowaua watu wako mwenyewe na kujitia unajisi kwa kufanya sanamu za miungu; kwa hiyo wakati wako wa adhabu umewadia.
4 Una hatia kutokana na damu uliyomwaga. Umejifanya najisi kwa sanamu ulizojifanyia. Siku yako ya adhabu umeileta karibu nawe; naam, siku zako zimehesabiwa. Ndio maana nimekufanya udhihakiwe na mataifa na kudharauliwa na nchi zote.
5 Nchi zote za mbali na karibu zitakudhihaki. Umejipatia sifa mbaya na kujaa fujo.
6 “Wakuu wa Israeli walioko kwako, kila mmoja kadiri ya nguvu zake huua watu.
7 Kwako baba na mama wanadharauliwa. Mgeni anayekaa kwako anapokonywa mali yake. Yatima na wajane wanaonewa.
8 Wewe umedharau vyombo vyangu vitakatifu na kuzikufuru sabato zangu.
9 Kwako wamo wanaowasingizia wengine ili wauawe. Wakazi wako hushiriki chakula kilichotolewa kwa miungu milimani. Watu wako wanatenda ufisadi.