2 “Wewe mtu! Watu wa Tiro wameucheka mji wa Yerusalemu na kusema: ‘Aha! Yerusalemu mji ambao watu wote walipita, umeangamizwa! Sasa umetuachia nafasi; utajiri wake umeharibiwa!’
3 Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa nitapambana nawe ewe Tiro. Nitazusha mataifa mengi dhidi yako, nao watakuja kama mawimbi ya bahari.
4 Wataziharibu kuta zako na kuibomoa minara yako. Nitafagilia mbali udongo wako na kukufanya kuwa jabali tupu.
5 Utakuwa mahali pakavu katikati ya bahari, na wavuvi watakausha nyavu zao hapo; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mataifa yatakuteka nyara,
6 na miji iliyo jirani nawe huko bara itaangamizwa. Nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu
7 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kutoka kaskazini nitamleta Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi, magari ya vita, wapandafarasi na jeshi kubwa, aje kukushambulia.
8 Ataiangamiza miji iliyo jirani nawe huko bara. Kisha atajenga kuta za kukushambulia, atajaza udongo kwenye kuta zako na kuweka ukuta wenye ngao ili kukushambulia.