11 Kisha nenda kwa watu wako waliopelekwa uhamishoni, ukawaambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Waambie hata kama watakusikiliza au watakataa kukusikiliza.”
12 Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama ya tetemeko kubwa. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu mbinguni.”
13 Pia nilisikia sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yalipokuwa yanagusana, pamoja na sauti ya mgongano wa yale magurudumu kandokando yao.
14 Basi, roho ya Mungu ikaninyanyua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na ukali rohoni mwangu, nao mkono wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa na nguvu juu yangu.
15 Nikawafikia wale watu waliokuwa uhamishoni, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari huko Tel-abibu. Nikakaa nao kwa muda wa siku saba nikiwa nimepigwa bumbuazi.
16 Baada ya siku saba, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
17 “Wewe mtu nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Kila utakaposikia neno kutoka kwangu utawaonya watu kwa niaba yangu.