14 “Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii na kumwambia Gogu kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati taifa langu la Israeli linaishi kwa usalama, wewe utafunga safari
15 kutoka kwenye maskani yako, huko mbali kabisa kaskazini, uje pamoja na watu wengi wakiwa wote wamepanda farasi: Jeshi kubwa na lenye nguvu.
16 Utawakabili Waisraeli, kama wingu linalotanda juu ya nchi. Wakati huo nitakutuma uishambulie nchi yangu, ili mataifa yajue kwamba nimekutumia wewe Gogu ili nioneshe utakatifu wangu mbele yao.
17 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, wewe ndiwe niliyesema habari zako hapo kale kwa njia ya watumishi wangu manabii wa Israeli, ambao walitabiri nyakati zile kuwa baadaye nitakuleta upambane na watu wa Israeli.”
18 Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku ile Gogu atakapoishambulia nchi ya Israeli, nitawasha ghadhabu yangu.
19 Mimi natamka rasmi kwa wivu na ghadhabu yangu kali kwamba siku hiyo kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini Israeli.
20 Samaki baharini na ndege warukao, wanyama wa porini, viumbe vyote vitambaavyo pamoja na watu wote duniani, watatetemeka kwa kuniona. Milima itaporomoshwa, magenge yataanguka na kuta zote zitaanguka chini.