9 Utakwenda kasi kama tufani na kuifunika nchi kama wingu, wewe mwenyewe na jeshi lako lote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe.
10 “Wewe Gogu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile itakapofika utaanza kuwaza moyoni mwako na kupanga mipango miovu na kusema:
11 ‘Nitakwenda kuishambulia nchi isiyo na kuta, nchi ambako wananchi wake wanaishi kwa amani. Wote wanakaa katika miji isiyo na kuta; hawana makomeo wala malango.’
12 Utapora na kuteka mali za watu wanaokaa katika miji ambayo ilikuwa jangwa. Watu hao wamekusanywa kutoka mataifa na sasa wana mifugo na mali; nao wanakaa kwenye kitovu cha dunia.
13 Wakazi wa Sheba na Dedani pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vitongoji vyake watakuuliza, ‘Je, umekuja kuteka nyara? Je, umekusanya jeshi lako ili kushambulia na kutwaa nyara na kuchukua fedha na dhahabu, mifugo na bidhaa, na kuondoka na nyara nyingi?’
14 “Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii na kumwambia Gogu kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati taifa langu la Israeli linaishi kwa usalama, wewe utafunga safari
15 kutoka kwenye maskani yako, huko mbali kabisa kaskazini, uje pamoja na watu wengi wakiwa wote wamepanda farasi: Jeshi kubwa na lenye nguvu.