23 Mataifa yatajua kuwa Waisraeli walikwenda uhamishoni kutokana na makosa yao wenyewe waliyonikosea. Waliniasi, nami nikageuka wasinione, nikawaweka mikononi mwa maadui zao wakauawa.
24 Niligeuka wasinione, nikawatenda kulingana na uchafu na makosa yao.
25 “Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa nitawahurumia Waisraeli wazawa wa Yakobo, na kuwarudishia fanaka yao. Daima nataka jina langu takatifu liheshimiwe.
26 Watakapokuwa wanaishi kwa usalama katika nchi yao, bila ya kutishwa, watasahau aibu yao na uasi walionitenda.
27 Wakati huo, nitakuwa nimewarudisha kutoka kwa mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za maadui zao na kudhihirisha utakatifu wangu mbele ya mataifa mengi.
28 Kisha watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, kwa sababu mimi niliwapeleka uhamishoni kati ya mataifa na kuwarudisha tena katika nchi yao. Sitamwacha hata mtu wao abaki miongoni mwa mataifa.
29 Nitakapowamiminia Waisraeli roho yangu, sitageuka tena wasinione. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”