1 Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye lango linaloelekea mashariki.
2 Utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea upande wa mashariki. Pamoja nao kulikuwapo mshindo wa kuja kwake kama mshindo wa maji mengi, nchi ilingaa kwa utukufu wake.
3 Maono hayo yalikuwa kama maono niliyoyaona Mungu alipokuja kuuangamiza mji wa Yerusalemu. Pia yalifanana na maono niliyoyaona karibu na mto Kebari. Nikaanguka kifudifudi.
4 Nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya lango la mashariki.
5 Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka kwenye uwanja wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
6 Yule mtu akiwa anasimama karibu nami, nilisikia mtu fulani akisema kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu;