13 “Vipimo vya matoleo yenu ya nafaka vitakuwa hivi: Moja ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano, na moja ya sita ya efa katika homeri moja ya shayiri.
14 Kiwango cha mafuta kitakuwa hivi: Moja ya bathi ya mafuta kutoka kila kori (kori moja ni sawa na homeri moja ambayo ni sawa na bathi kumi).
15 Watatoa kondoo mmoja kwa kila kundi la kondoo 200 katika jamaa za Israeli. Wataleta sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, ili wapate kufanyiwa upatanisho. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
16 Watu wote nchini watampa sadaka hizo mtawala wa Israeli.
17 Itakuwa ni wajibu wa mtawala kuhakikisha kuwa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zinazotolewa wakati wa sikukuu, mwezi mwandamo, sabato, na sikukuu zozote zilizowekwa zinapatikana kwa Waisraeli. Mtawala mwenyewe ataandaa sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani ili kuwafanyia upatanisho watu wote wa Israeli.
18 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mtatambika fahali mdogo asiye na dosari ili kutakasa maskani yangu.
19 Kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuipaka miimo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kona za madhabahu, na miimo ya nafasi ya kuingilia kwenye ua wa ndani.