1 Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilikuwa nyumbani kwangu pamoja na wazee wa Yuda. Basi, ghafla nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu.
2 Nilipotazama, nikaona maono: Kitu kilichofanana na binadamu. Sehemu yake ya chini, iliyoonekana kama ndio kiuno chake, ilikuwa kama moto. Toka kiuno chake kwenda juu alikuwa na mngao kama wa shaba ingaayo.
3 Basi, akanyosha kitu kama mkono, akanishika kwa nywele zangu. Roho ya Mungu ikaninyanyua kati ya ardhi na mbingu, ikanipeleka mpaka Yerusalemu nikiwa katika maono hayo ya Mungu. Nikafika kwenye kiingilio cha lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa kaskazini, mahali palipowekwa sanamu iliyomchukiza Mungu.
4 Utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo; nao ulikuwa kama utukufu ule niliouona katika maono kule bondeni.
5 Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, tazama upande wa kaskazini.” Nami nikatazama upande wa kaskazini, na huko upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, niliona ile sanamu iliyomchukiza Mungu.