2 Watu sita wakaja kutoka upande wa lango la juu linaloelekea kaskazini, kila mmoja na silaha yake ya kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao, alikuwapo mtu mmoja ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kitani, naye ana kidau cha wino. Wakaingia ndani ya hekalu, wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba.
3 Kisha utukufu wa Mungu wa Israeli uliondoka pale juu ya kiumbe chenye mabawa na kupanda juu mpaka kizingiti cha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino,
4 akamwambia, “Pita katikati ya mji wa Yerusalemu, ukatie alama kwenye vipaji vya nyuso za watu wanaohuzunika na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.”
5 Kisha akawaambia wale wengine mimi nikiwa nasikia, “Piteni mjini mkimfuata, mkaue watu; msimwachie yeyote wala msiwe na huruma.
6 Waueni wazee papo hapo, wavulana kwa wasichana, watoto na wanawake; lakini kila mmoja mwenye alama, msimguse. Anzeni katika maskani yangu.” Basi, wakaanza na wazee waliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
7 Akawaambia, “Tieni unajisi nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa kuzijaza nyua zake maiti. Songeni mbele.” Basi, wakaenda, wakawaua watu mjini.
8 Wakati walipokuwa wakiwaua, mimi niliachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikalia, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utaangamiza watu wote wa Israeli waliobaki, ukitimiza ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?”