7 Basi, maofisa wa Moabu na Midiani wakachukua ada ya mwaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balaamu. Walipowasili, walimpa Balaamu ujumbe wa Balaki.
8 Balaamu akawaambia, “Laleni huku usiku huu, nami nitawajulisheni atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balaamu.
9 Kisha Mungu alimjia Balaamu, akamwuliza, “Ni nani hawa wanaokaa nawe?”
10 Balaamu akamjibu Mungu, “Balaki mwana wa Sipori amenipelekea ujumbe kwamba
11 kuna watu wa taifa fulani waliotoka Misri, nao wameenea kila mahali nchini. Ameniomba niende kuwalaani watu hao ili pengine afaulu kupigana nao na kuwafukuza.”
12 Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.”
13 Basi, asubuhi yake Balaamu aliamka, akawaambia maofisa wa Balaki, “Rudini nchini mwenu, kwa maana Mwenyezi-Mungu hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.”