22 Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati na madini ya risasi,
23 yaani vitu vyote ambavyo vinastahimili moto, vitatakaswa kwa kupitishwa motoni. Hata hivyo, ni lazima vitakaswe kwa maji ya utakaso. Vitu vingine vyote ambavyo haviwezi kustahimili moto vitatakaswa kwa maji ya utakaso.
24 Siku ya saba ni lazima muyafue mavazi yenu; ndipo mtakapokuwa safi na kuruhusiwa kuingia kambini.”
25 Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia,
26 “Wewe na kuhani Eleazari, pamoja na viongozi wa koo za jumuiya ya Waisraeli, fanyeni hesabu ya nyara ya vitu, watu na wanyama.
27 Gaweni nyara katika mafungu mawili, fungu moja la wanajeshi waliokwenda vitani na fungu lingine kwa ajili ya jumuiya nzima.
28 Kisha kutokana na lile fungu la wanajeshi waliokwenda vitani, tenga zaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu: Kitu kimoja kutoka kila vitu 500, iwe ni watu, ng'ombe, punda, kondoo au mbuzi,