2 “Wahesabu watu wa ukoo wa Kohathi, mmoja wa koo za Lawi, kufuatana na jamaa zao na koo zao;
3 utawaorodhesha wanaume wote wenye umri kati ya miaka thelathini na hamsini wanaofaa kujiunga na huduma ya hema la mkutano.
4 Hii ndio itakayokuwa huduma ya wana wa Kohathi, kuhusu vitu vitakatifu kabisa.
5 “Wakati wa kuvunja kambi, Aroni na wanawe wataingia katika hema, na kulishusha pazia lililoko mbele ya sanduku la agano, kisha walifunike kwa pazia hilo.
6 Juu yake wataweka kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi, kisha watatandaza kitambaa cha rangi ya buluu safi. Halafu wataingiza mipiko ya kulichukulia sanduku hilo.
7 “Juu ya meza ya kutolea mikate inayowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu watatandaza kitambaa cha buluu ambacho juu yake wataweka sahani, visahani vya ubani, bakuli na bilauri, kwa ajili ya kutolea tambiko za kinywaji. Daima kutakuwa na mkate juu ya meza.
8 Kisha, watavifunika vyombo hivi vyote kwa kitambaa chekundu, na juu yake wataweka kifuniko cha ngozi laini ya mbuzi. Halafu wataingiza mipiko yake ya kulibeba.