4 Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako.
5 Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani.
6 Nzige hao watajaa katika nyumba zako, nyumba za maofisa wako na za Wamisri wote; watakuwa wengi kiasi ambacho hata wazee wenu hawajapata kuona tangu walipozaliwa, hadi leo.’” Basi, Mose akatoka kwa Farao.
7 Viongozi wa Farao wakamwuliza, “Je, mtu huyu atatusumbua mpaka lini? Waache watu hawa waende zao wakamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Je, hujali kwamba nchi ya Misri inaangamia?”
8 Hapo, Mose na Aroni wakaitwa warudi kwa Farao, naye akawaambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini, nauliza: Ni kina nani watakaokwenda pamoja nanyi?”
9 Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.”
10 Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu.