9 Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.”
10 Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu.
11 La hasha! Ni wanaume tu watakaokwenda kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana hilo ndilo mnalotaka.” Hapo Mose na Aroni wakafukuzwa mbele ya Farao.
12 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige watokee ili waingie na kula mimea yote nchini na vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.”
13 Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige.
14 Hao nzige wakaenea kila mahali nchini Misri, wakatua juu ya ardhi yote. Nzige hao walikuwa kundi kubwa kupindukia, kiasi ambacho hakijapata kutokea wala hakitatokea tena.
15 Waliifunika nchi yote ya Misri, hata ardhi ikaonekana kuwa giza. Walikula mimea yote na matunda yote yaliyosalia wakati wa ile mvua ya mawe. Hakuna hata jani moja lililosalia nchini. Hakuna jani lolote lililosalia juu ya miti wala mimea popote katika nchi yote ya Misri.