6 Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu.
7 Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi.
8 Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema.
9 Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye.
10 Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake.
11 Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani.
12 Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako.