10 Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kufanya kama walivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Aroni aliitupa fimbo yake chini mbele ya Farao na maofisa wake, nayo ikawa nyoka.
11 Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao.
12 Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao.
13 Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.
14 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Moyo wa Farao umekuwa mgumu. Anakataa kuwaacha Waisraeli waondoke.
15 Basi, nenda ukakutane naye kesho asubuhi, wakati anapokwenda mtoni Nili. Mngojee kando ya mto. Chukua mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka.
16 Kisha mwambie hivi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma kwako, naye asema hivi, ‘Waache watu wangu waende zao ili wanitumikie jangwani, lakini mpaka sasa wewe hupendi kutii.