8 Kisha Farao akamwita Mose na Aroni, akamwambia, “Msihi Mwenyezi-Mungu, ili aniondolee mimi na watu wangu vyura hawa, nami nitawaacha Waisraeli waende zao na kumtambikia Mwenyezi-Mungu.”
9 Mose akamjibu Farao, “Haya! Waweza kutaja wakati unaotaka nikuombee kwa Mungu, niwaombee maofisa wako na watu wako; nitamwomba awaangamize vyura hawa waliomo katika nyumba zenu; watabaki tu mtoni Nili!”
10 Farao akamwambia, “Kesho.” Mose akasema, “Nitafanya kama unavyosema, ili ujue kwamba hakuna yeyote anayelingana na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
11 Vyura wataondoka kwako, na kwenye nyumba zenu, kwa maofisa wako na kwa watu wako; watabaki tu katika mto Nili.”
12 Basi, Mose na Aroni wakaondoka nyumbani kwa Farao, na Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu amwondolee Farao uvamizi wa vyura hao aliomletea.
13 Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba: Vyura wakafa majumbani, viwanjani na kwenye kumbi za nyumba na katika mashamba.
14 Watu wakawakusanya vyura hao marundo marundo; nchi nzima ikanuka.