10 Hili ndilo agano utakaloshika kati yangu na wewe na wazawa wako: Kila mwanamume miongoni mwenu lazima atahiriwe.
11 Mtatahiriwa kwa kukata magovi yenu, na hii itakuwa ndiyo alama ya agano kati yangu nanyi.
12 Kila mtoto wa kiume wa siku nane miongoni mwenu ni lazima atahiriwe. Kila mwanamume katika vizazi vyenu, awe mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwenu au aliyenunuliwa kwa fedha zenu kutoka kwa mgeni asiye mzawa wako;
13 naam, kila mmoja wao aliyezaliwa katika nyumba yako na hata aliyenunuliwa kwa fedha zako ni lazima atahiriwe. Hiyo ni alama ya agano langu katika miili yenu, agano la milele.
14 Mwanamume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, kwani atakuwa amevunja agano langu.”
15 Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kuhusu mkeo, hutamwita tena jina lake Sarai, bali jina lake litakuwa Sara.
16 Nitambariki, naye atakuzalia mtoto wa kiume. Naam, nitambariki Sara, naye atakuwa mama wa mataifa mengi na wafalme wa mataifa watatoka kwake.”