7 Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko.
8 Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.”
9 Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo.
10 Kisha, huyo mtumishi akachukua ngamia kumi wa bwana wake akaondoka akiwa na zawadi nzuri za kila aina. Akasafiri kwenda katika mji alimokaa Nahori, nchini Mesopotamia.
11 Alipowasili, aliwapigisha magoti ngamia wake kando ya kisima kilichokuwa nje ya mji. Ilikuwa jioni wakati ambapo wanawake huenda kisimani kuteka maji.
12 Naye akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba unijalie nifaulu leo na umfadhili Abrahamu bwana wangu.
13 Niko hapa kando ya kisima ambapo binti za wenyeji wa mji huja kuteka maji.