1 Basi, Yakobo alitazama, akamwona Esau akija pamoja na watu 400. Hapo, akawagawa watoto wake kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wawili.
2 Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Raheli na mwanawe Yosefu.
3 Kisha yeye mwenyewe akawatangulia, akaenda akiinama mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake.
4 Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia.
5 Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.”