8 Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.”
9 Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.”
10 Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa.
11 Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.
12 Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.”
13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa.
14 Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.”