13 Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.”
14 Basi, Farao akaamuru Yosefu aitwe; naye akatolewa gerezani haraka. Baada ya kunyoa na kubadili nguo zake, Yosefu akaja mbele ya Farao.
15 Farao akamwambia Yosefu, “Mimi nimeota ndoto, lakini hakuna mtu aliyeweza kunitafsiria. Nimesikia sifa zako kwamba wewe ukiambiwa ndoto unaweza kuitafsiri.”
16 Yosefu akamjibu Farao, “Sina uwezo huo; lakini Mungu atakupa jibu lifaalo.”
17 Hapo Farao akamwambia Yosefu, “Niliota kwamba nimesimama kando ya mto Nili,
18 nikaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi.
19 Hao wakafuatwa na ng'ombe wengine saba dhaifu, wembamba na wamekonda sana. Mimi sijapata kamwe kuona ng'ombe wa hali hiyo katika nchi ya Misri.