43 Farao akampandisha katika gari lake la pili la farasi na walinzi wakatangulia mbele ya Yosefu wakipaza sauti na kusema, “Pigeni magoti!” Ndivyo Farao alivyompa Yosefu madaraka makubwa juu ya nchi yote ya Misri.
44 Zaidi ya hayo, Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ndimi Farao! Nasema: Mtu yeyote katika nchi nzima ya Misri asiinue mkono wala mguu wake bila kibali chako.”
45 Farao akampa Yosefu jina la Kimisri: Safenath-panea. Akamwoza Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni. Basi, Yosefu akaanza kuitembelea nchi nzima ya Misri.
46 Yosefu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kumtumikia Farao, mfalme wa Misri. Alitoka nyumbani kwa Farao na kuitembelea nchi yote ya Misri.
47 Ikawa, katika miaka ile saba ya shibe, mashamba ya Misri yakatoa mazao kwa wingi sana.
48 Yosefu akakusanya chakula chote wakati huo wa miaka saba ya shibe na kukiweka akiba katika miji ya Misri. Katika kila mji akaweka akiba ya chakula kutoka mashamba yaliyo karibu na mji huo.
49 Yosefu akaweka akiba ya nafaka kwa wingi mno ikawa nyingi kama mchanga wa bahari, hata isiweze kupimika.