11 Basi, Yosefu akawapa baba yake na ndugu zake eneo la Ramesesi lililo bora kabisa katika nchi ya Misri, liwe makao yao, nao wakalimiliki kama alivyoagiza Farao.
12 Yosefu akawa anawapatia chakula baba yake, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake kulingana na idadi ya watu waliowategemea.
13 Baadaye chakula kiliadimika kabisa nchini kote. Njaa ilikuwa kali sana hata ikawafanya watu wote katika nchi ya Misri na ya Kanaani kudhoofika.
14 Yosefu akakusanya fedha yote ya nchi ya Misri na Kanaani kutokana na nafaka waliyonunua, akaipeleka fedha hiyo ikulu kwa Farao.
15 Baada ya watu wote wa nchi ya Misri na Kanaani kutumia fedha yao yote Wamisri wote walimjia Yosefu na kumwambia, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Tazama, sasa fedha yetu imekwisha!”
16 Yosefu akawaambia, “Kama fedha yenu imekwisha, basi nipeni mifugo yenu, nami nitawapa nafaka.”
17 Ndipo wakamletea Yosefu mifugo yao: Farasi, ng'ombe, kondoo, mbuzi na punda, naye akawapa chakula. Mwaka huo Yosefu akawa anawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.