12 Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza:
13 Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia.
14 Baada ya kumzika baba yake, Yosefu alirudi Misri pamoja na ndugu zake na watu wote waliokuwa wameandamana naye kwenda kumzika baba yake.
15 Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.”
16 Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi,
17 ‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia.
18 Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.”