7 Basi, Yosefu akaondoka kwenda kumzika baba yake akifuatana na watumishi wote wa Farao, wazee wa nyumba ya Farao, pamoja na wazee wa nchi nzima ya Misri.
8 Hali kadhalika, Yosefu alifuatana na jamaa yake yote, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake Yakobo. Katika eneo la Gosheni walibaki watoto wao tu pamoja na kondoo, mbuzi na ng'ombe wao.
9 Pia waliandamana naye wapandafarasi na magari; lilikuwa kundi kubwa sana.
10 Walipofika katika uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, ngambo ya mto Yordani, waliomboleza kwa huzuni kubwa, naye Yosefu akamfanyia baba yake marehemu matanga ya siku saba.
11 Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo, walipoyaona maombolezo yaliyofanywa kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, wakasema, “Maombolezo haya ya Wamisri, kweli ni makubwa!” Kwa hiyo, mahali pale pakaitwa Abel-misri, napo pako ngambo ya mto Yordani.
12 Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza:
13 Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia.