11 Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12 Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku.
13 Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina.
14 Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina.
15 Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai.
16 Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa.
17 Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi.