12 “Sasa waulize hao watu waasi kama wanaelewa maana ya mfano huo. Waambie kuwa, mfalme wa Babuloni alikuja Yerusalemu, akamwondoa mfalme na viongozi wake, akawapeleka Babuloni.
13 Kisha akamtawaza mmoja wa jamaa ya kifalme, akafanya naye mapatano, akamwapisha. Aliwaondoa humo nchini watu mashujaa akawapeleka mbali
14 ili utawala huo uwe dhaifu na uzingatie agano lake mfalme wa Babuloni.
15 Lakini yule mfalme mpya alimwasi mfalme wa Babuloni kwa kuwatuma wajumbe Misri kuomba farasi na askari wengi. Je, mfalme huyo atafaulu? Je, anayefanya hivyo na kuvunja agano lake ataweza kuepa adhabu?
16 “Mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, kama niishivyo, mfalme huyu atafia katika nchi ya Babuloni, nchi ya mfalme yule aliyemweka awe mfalme, na ambaye amedharau kile kiapo na kuvunja lile agano alilofanya naye.
17 Hakika, Farao pamoja na jeshi lake kubwa hataweza kumsaidia vitani wakati Wababuloni watakapomzungushia ngome na kuta ili kuwaua watu wengi.
18 Kwa kuwa alikidharau kile kiapo na kuvunja lile agano ambalo aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na kufanya mambo haya yote, hakika hataokoka.