13 Ewe Yerusalemu, matendo yako machafu yamekutia unajisi. Ingawa nilijaribu kuutakasa, wenyewe ulibaki najisi. Basi, hutatakasika tena mpaka nitakapoitosheleza hasira yangu juu yako.
14 Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Jambo hilo litakamilika; mimi nitalitenda. Sitaghairi jambo hilo wala kukuonea huruma. Nitakuadhibu kulingana na mwenendo na matendo yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
15 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
16 “Wewe mtu! Tazama, kwa pigo moja nitakuondolea mpenzi wako. Lakini usiomboleze, wala kulia, wala kutoa machozi.
17 Utasononeka, lakini sio kwa sauti. Hutamfanyia matanga huyo aliyekufa. Vaa viatu vyako na kuvaa kilemba; usiufunike uso wako wala kula chakula cha matanga.”
18 Basi, asubuhi nilizungumza na watu, na jioni mke wangu akafariki. Na kesho yake asubuhi, nilifanya kama nilivyoamriwa.
19 Watu wakaniuliza: “Je, jambo hili unalofanya lamaanisha nini kwetu?”