6 “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mji huo ni kama chungu chenye kutu, ambacho kutu yake haiwezi kutoka! Vipande vya nyama ndani yake hutolewa kimojakimoja bila kuchaguliwa.
7 Mauaji yamo humo mjini; damu yenyewe haikumwagwa udongoni ifunikwe na vumbi, ila ilimwagwa mwambani.
8 Damu hiyo nimeiacha huko mwambani ili isifunikwe, nipate kuamsha ghadhabu yangu na kulipiza kisasi.
9 “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mimi nitarundika rundo kubwa la kuni.
10 Nitaleta magogo ya kuni na kuwasha moto. Nitachemsha nyama vizuri sana. Nitachemsha na kukausha mchuzi, na mifupa nitaiunguza!
11 Hicho chungu kitupu nitakiweka juu ya makaa kipate moto sana, shaba yake ipate moto, uchafu wake uyeyushwe na kutu iunguzwe.
12 Lakini najisumbua bure; kutu yake nene haitoki hata kwa moto.