4 Halafu ghafla, Mwenyezi-Mungu akawaambia Mose, Aroni na Miriamu, “Njoni katika hema la mkutano, nyinyi watatu.” Basi, wote watatu wakaenda kwenye hema la mkutano.
5 Hapo Mwenyezi-Mungu akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye mlango wa hema, akawaita Aroni na Miriamu. Wote wawili wakasogea mbele.
6 Kisha Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu: Kama kuna nabii miongoni mwenu, mimi Mwenyezi-Mungu hujifahamisha kwake katika maono na kuongea naye katika ndoto.
7 Lakini kumhusu mtumishi wangu Mose, hali ni tofauti kabisa. Yeye ana jukumu la kuwatunza watu wangu wote.
8 Mimi huongea naye ana kwa ana, waziwazi na si kwa kutumia mafumbo. Yeye huliona umbo langu mimi Mwenyezi-Mungu. Kwa nini, basi, hamkuogopa kusema vibaya dhidi ya mtumishi wangu Mose?”
9 Hapo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi yao, akaondoka, akaenda zake.
10 Wingu lilipoondoka juu ya hema la mkutano, Miriamu alionekana ana ukoma, mweupe kama theluji. Aroni alipogeuka na kumtazama Miriamu, alishangaa kuona kuwa ameshikwa na ukoma.