34 Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.”
35 Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.
36 Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu.
37 Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?”
38 Balaamu akamjibu Balaki, “Sasa nimekuja! Lakini, je, nina mamlaka ya kusema chochote tu? Jambo atakaloniambia Mungu ndilo ninalopaswa kusema.”
39 Basi, Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika mjini Kiriath-husothi.
40 Huko Balaki alitoa kafara ya ng'ombe na kondoo, akawagawia nyama Balaamu na maofisa waliokuwa pamoja naye.