1 Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa kisha uniletee fahali saba na kondoo madume saba.”
2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema. Basi, wakatoa juu ya kila madhabahu kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja.
3 Halafu Balaamu akamwambia Balaki, “Baki hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami niende. Labda Mwenyezi-Mungu atakutana nami. Chochote atakachonionesha nitakuja kukuambia.” Basi, Balaamu akaenda peke yake juu ya kilele cha mlima.
4 Mungu akakutana naye. Balaamu akamwambia, “Nimetayarisha madhabahu saba na kutoa kafara fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.”
5 Mwenyezi-Mungu akampa Balaamu maneno atakayosema na kumwambia arudi kwa Balaki.
6 Balaamu akarudi, akamkuta Balaki amesimama palepale karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, pamoja na maofisa wote wa Moabu.
7 Balaamu akamtolea Balaki kauli yake, akasema,“Balaki amenileta hapa kutoka Aramu,naam, mfalme wa Moabu amenileta kutoka milima ya mashariki.‘Njoo uwalaani watu wa Yakobo kwa ajili yangu,naam, njoo uwalaumu Waisraeli!’