37 Pia walihitajika kutunza nguzo za ua zilizouzunguka na vitako vyake, vigingi na kamba zake.
38 Mose na Aroni na wana wao walitakiwa kupiga kambi yao mbele ya hema takatifu upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua. Wajibu wao ulikuwa kutoa huduma kwenye mahali patakatifu kwa lolote lililohitajika kufanyika kwa ajili ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyesogea karibu ilibidi auawe.
39 Idadi ya Walawi kulingana na familia zao, wanaume wote kuanzia watoto wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ambao Mose na Aroni waliwahesabu kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ilikuwa watu 22,000.
40 Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wahesabu kwa majina wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wa Waisraeli kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi.
41 Nawe utatenga Walawi kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu; pia utatenga kwa ajili yangu mifugo yote ya Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo ya watu wa Israeli.”
42 Basi, Mose akawahesabu wazaliwa wa kwanza wote wa watu wa Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.
43 Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume kadiri ya hesabu ya majina, kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi, kufuata walivyohesabiwa, walikuwa 22,273.