14 “Ikiwa kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi na anapenda kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu huyo sharti afanye hivyo kulingana na masharti na maagizo yote ya Pasaka. Kila mtu atafuata masharti yaleyale, akiwa mgeni au mwenyeji.”
15 Siku ambayo hema takatifu lilisimikwa, wingu lilishuka na kulifunika hema la maamuzi. Wakati wa usiku wingu hilo lilionekana kama moto mpaka asubuhi.
16 Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku; wingu lililifunika hema mchana, na usiku lilionekana kama moto.
17 Kila mara wingu hilo lilipoinuliwa juu ya hema, Waisraeli walivunja kambi na kupiga kambi tena mahali wingu hilo lilipotua.
18 Walisafiri kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, na kupiga kambi tena kwa amri yake. Muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, watu walikaa katika kambi hiyo.
19 Hata kama wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku nyingi, Waisraeli walimtii Mwenyezi-Mungu, nao hawakuondoka.
20 Wakati mwingine wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku chache tu; lakini kila wakati Waisraeli walibaki kambini; walihama kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru.