12 Kila mtoto wa kiume wa siku nane miongoni mwenu ni lazima atahiriwe. Kila mwanamume katika vizazi vyenu, awe mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwenu au aliyenunuliwa kwa fedha zenu kutoka kwa mgeni asiye mzawa wako;
13 naam, kila mmoja wao aliyezaliwa katika nyumba yako na hata aliyenunuliwa kwa fedha zako ni lazima atahiriwe. Hiyo ni alama ya agano langu katika miili yenu, agano la milele.
14 Mwanamume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, kwani atakuwa amevunja agano langu.”
15 Kisha Mungu akamwambia Abrahamu, “Kuhusu mkeo, hutamwita tena jina lake Sarai, bali jina lake litakuwa Sara.
16 Nitambariki, naye atakuzalia mtoto wa kiume. Naam, nitambariki Sara, naye atakuwa mama wa mataifa mengi na wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
17 Hapo Abrahamu akasujudu, akacheka moyoni mwake akiwaza, “Ati, itawezekana kweli mtoto kuzaliwa kwa mzee wa miaka 100? Na je, Sara ambaye umri wake ni miaka tisini, ataweza kupata mtoto?”
18 Basi, Abrahamu akamwambia Mungu, “Laiti ungekubali ahadi yako hiyo imhusu Ishmaeli.”